Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amevionya vyama vya ushirika nchini, kuwa sekta hiyo si sehemu ya kujinufaisha na badala yake, viongozi wawatumikie wanachama wao ipasavyo ili kuwaletea maendeleo.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kijiji cha Chomachankola mkoani Tabora, Majaliwa amesema serikali itachukua hatua kali dhidi ya viongozi wa ushirika watakaojihusisha katika ubadhilifu na kuwaasa kufanya kazi kwa uaminifu.
Waziri Mkuu pia amewataka viongozi wa Chama cha Ushirika Tabora (Ingembensambo) kuwasaidia wakulima/wanachama wa chama hicho kupata bima ya afya itakayowasaidia kupunguza gharama za matibabu kwasababu shirika la bima ya afya limeshaanza kutoa huduma kwa wakulima ambapo kila mwanachama atahitaji kulipa Tsh. 75,000 kwa mwaka itakayotumia kutibu mwenza wake pamoja na watoto wanne katika hospitali mbalimbali nchini ikiwemo hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Soma Pia Viongozi wa ushirika matatani kwa ubadhirifu
Aidha Majaliwa ametoa wito kwa wakulima wa zao la pamba kuzalisha kwa wingi msimu ujao kutokana na uwepo wa soko la uhakika. Akisisitiza kuhusu uzalishaji wa zao la pamba, Majaliwa amesema kuwa tayari kuna viwanda vya kuchambua pamba vilivyoanzishwa nchini na tayari wamiliki wa viwanda hivyo wamekuwa wakilalamika kukosa malighafi hiyo.
Soma Pia Wakulima wa mpunga washauriwa kuunda ushirika
Waziri Mkuu pia ameshauri vijana wa mkoani humo kuachana na tabia ya kushinda vijiweni wakicheza ‘Pool’ na badala yake, wajikite katika uzalishaji wa kilimo cha pamba ili kupiga vita umaskini na utegemezi.