Home BIASHARAUWEKEZAJI Iringa yajikita kwenye viwanda

Iringa yajikita kwenye viwanda

0 comment 76 views

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ally Hapi amesema serikali mkoani humo imejikita katika kuimarisha uchumi wa viwanda, ikiwa ni moja ya azma kuu inayohitaji kutekelezwa katika serikali ya awamu ya tano,kwa kuhakikisha inaandaa mazingira rafiki kwa ajili ya wawekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu bora itakayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza mkoani humo.

Hapi amesema hayo alipokutana na wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vikubwa na vidogo mkoani humo  ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu uteuzi uliofanyika hivi karibuni na Rais Magufuli.

Soma Pia FAO kuwawezesha wakulima

Hapi amesema licha ya serikali kufanya juhudi kuboresha mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara ni vyema pia wafanyabiashara hao wakatambua kuwa wana wajibu wa kulipa kodi kwa wakati, kuwapa wafanyakazi mkataba wa kazi pamoja na kuwajengea makazi watumishi wao. Hapi amewataka pia wafanyabiashara mkoani humo kujenga viwanda vikubwa vya kusaga nafaka kutokana na mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa zao la mahindi, na kusisitiza kuwa fursa hiyo itasaidia kukuza soko la zao ambapo badala ya kusafirisha mahindi mikoa na nchi jirani wataanza kuja kununua unga.

Aidha ameitaka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuweka miundombinu karibu na mazingira ambapo uwekezaji wa viwanda utafanyika kwa lengo la kuwavutia wawekezaji.

Soma Pia Serikali yataka wawekezaji kufuata sheria

Akizungumzia kuhusu hali ya mkoa huo, Ally Hapi amesema kuwa asilimia 75 ya ardhi ya mkoa huo inafaa kwa ajili ya kilimo na asilimia kubwa ya malighafi za viwanda hivyo inatoka  katika kilimo, hivyo ameshauri wakulima na wawekezaji kuendelea kuongeza nguvu katika uzalishaji ili kuongeza pato la taifa sambamba na kuliingizia taifa fedha za kigeni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah ameiomba Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na Shirika la Maendeleo ya viwanda Vidogo (SIDO) kushirikiana na wenye viwanda kujua mahitaji yao ili kuzalisha wataalamu watakaoendana na uhitaji wa huduma zilizopo.

 

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter