Dodoma ni moja kati ya miji inayokuwa kwa kasi ukilinganisha na miji mingine Tanzania. Hatua hii inatokana na serikali kuweka nguvu zaidi katika jiji hilo baada ya kuhamishia rasmi makao makuu ya nchi pamoja na tamko lililotolewa na Rais John Magufuli Aprili 26 mwaka huu kuupandisha hadhi mji huo kuwa jiji. Dodoma ni moja kati ya miji inayopatikana katikati ya nchi ya Tanzania ikiwa imezungukwa na vitu vingi na vya kipekee vinavyofanya watu wengi kuwekeza fursa mbalimbali za kiuchumi.
Soma Pia Ujenzi kuajiri 500 Dodoma
Ripoti iliyotolewa tarehe 24 Juni 2018 na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma imeonyesha jiji hilo likiongoza kwa ukusanyaji mapato ikifuatiwa na Dar es salaam.
Watu wengi watajiuliza maswali mengi hasa kuhusiana na fursa za kiuchumi zinazopatikana Jijini hapo kiasi cha kuzidi kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato ukilinganisha na mikoa pamoja na majiji mengine.
Zipo fursa mbalimbali zinazoifanya Dodoma kuzidi kufanya vizuri kiuchumi licha ya kuwa haina viwanda vingi kama Dar es salaam, lakini pia haina fursa nyingi za kiutalii ukilinganisha na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Uwepo wa Bunge. Dodoma ndio mji liliko Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo ni dhahiri kuwa kipindi cha vikao vya bunge wafanyabiashara na wajasiriamali wa mji huo wanafaidika kwa kiasi kikubwa sana katika kujiingizia kipato. Baadhi ya maeneo yanayowapatia wakazi wa maeneo hayo fedha kipindi cha vikao hivyo ni pamoja na wamiliki wa hoteli, migahawa, nyumba za kulala wageni, maduka ya nguo sambamba na wauzaji wa nafaka.
Uwepo wa Ofisi nyingi za Kiserikali na Kisiasa. Dodoma ni moja ya miji yenye ofisi nyingi za serikali. Ofisi hizi hazijaja tu kipindi hiki ambacho serikali ya awamu ya tano imehamishia makao makuu jijini hapo bali zilikuwepo toka muda. Hivyo ongezeko la wafanyakazi katika mji huo ni fursa nyingine ya kiuchumi kutokana na wizara zote kuhamishia ofisi zake.
Soma Pia Dodoma yashika namba moja ukusanyaji wa mapato
Uwepo wa Chuo Kikuu cha Dodoma. Dodoma ndio chuo pekee chenye idadi kubwa ya udahili katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa jangwa la Sahara kikitajwa kuwa na vitivo nyingi ukilinganisha na vyuo vingine. Chuo hiki kimeweza kuibua fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za usafiri, chakula, upanuzi wa makazi ya kuishi, maduka ya nguo na vifaa, migahawa n.k. Idadi kubwa ya wanafunzi jijini humo imeibua fursa mbalimbali za kiuchumi.
Kilimo cha Zabibu. Kuna usemi kuwa kama umefika Dodoma haujala zabibu basi haujafika. Ukizungumzia kilimo cha zabibu basi unazungumzia Dodoma. Zabibu ni moja kati ya fursa za kiuchumi zinazoifanya Dodma kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato kutokana na uzalishaji wa kutosha wa matunda hayo mabyo yamekuwa yakitumika pia kutengenezea juisi, mvinyo na dawa za binadamu.
Viwanda. Dodoma ina viwanda mbalimbali, moja ya viwanda vinavyoitambulisha Dodoma ni pamoja na kiwanda cha magodoro ya Dodoma (QFL) pamoja na kiwanda cha kusindika mvinyo wa zabibu cha Alko Vintages. Viwanda hivi vimekuwa ni chachu ya maendeleo ya Dodoma kutokana na kuzalisha bidhaa zake kwa wingi tena kwa ubora unaoaminika na Shrikia la Viwango vya Ubora Tanzania (TBS).
Kama hujafikiria kuhusu jiji hili na unahitaji kuwekeza, Dodoma ni sehemu salama kwa uwekezaji kutokana na uwepo wa ulinzi wa kutosha, fursa mbalimbali za kimaendeleo, ofisi za kiserikali, huduma mbalimbali za kibenki na idadi ya watu yenye kuridhisha hivyo uwekezaji wowote jijini humo umewekewa mazingira mazuri ya kufanikiwa.