Katika kuhakikisha huduma za usafiri wa anga zinazidi kuboreshwa kila siku. Shirika la ndege la Precision Air linalofanya shughuli zake katika mikoa mbalimbali ndani na nje ya nchi limeazimia kuanzisha safari mpya kwenda Chato na makao makuu ya nchi Dodoma ili kuendelea kupanua wigo na kuwahudumia wateja wake.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa shirika hilo, Hillary Mremi ambaye amedai Precision Air imegundua kuna fursa ya kutanua soko lake kupitia safari hizo na kuongeza kuwa, tayari shirika hilo limeshaanza kufanya tathmini katika maeneo hayo ili kutoa huduma zitakazoendana na uhitaji.
“Kumekuwa na matukio muhimu katika maeneo haya, kwa upande mmoja hatua ya serikali kuhamia Dodoma ni dhahiri itaongeza safari za watu kwenda na kutoka Dodoma.Precision kama shirika linaloongoza kwa kuwa na mtandao bora wa safari na shirika pekee la ndege ambalo ni mwanachama wa IATA nchini Tanzania tumedhamiria kuanzisha safari za Dodoma ili kuwawezesha wateja wetu wanaosafiri kupitia mtandao wetu mpana wa safari kuunganisha safari zao kwenda Dodoma”. Amesema Mremi.
Akifafanua kuhusu safari ya Chato, Mremi amesema ujenzi wa uwanja mpya katika mji huo umetoa fursa ya kuanzisha safari za ndege kanda ya ziwa na hivyo shirika limeichukulia kama fursa kujitanua. Katika hatua nyingine, Mremi ameipongeza serikali kwa hatua kubwa inazochukua kuboresha na kujenga miundombinu ya usafiri wa ndege akisisitiza ujenzi huo umekuwa ukichangia maendeleo ya nchi na kukuza uchumi kwa ujumla.