Home BIASHARAUWEKEZAJI Stiegler’s Gorge kusaidia utunzaji mazingira

Stiegler’s Gorge kusaidia utunzaji mazingira

0 comment 119 views

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji, Stiegler’s Gorge utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti uharibifu wa mazingira hapa nchini. Majaliwa amesema hayo baada ya kutembelea eneo utakapojengwa mradi huo na kueleza kuwa umeme huo utazalishwa kwa gharama nafuu na utakuwa wa uhakika zaidi.

Waziri Mkuu amedai kuwa kwa vile umeme utakaozalishwa katika mradi wa Stiegler’s Gorge utakuwa nafuu na hivyo kuwafikia wananchi wa kipato cha chini, utatumika kama nishati mbadala kwa kuni na mkaa ili kuepuka uharibifu wa mazingira hasa ukataji miti. Aidha, Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa serikali pamoja na vyama vya siasa kuwaelimisha wananchi kuhusu mradi wa Stiegler’s Gorge na faida zake kubwa kwa taifa kiuchumi. Waziri Mkuu pia amechukua nafasi hiyo kuwahakikishia watanzania kuwa mradi huo utajengwa na kukamilika katika muda uliokusudiwa.

Kuhusu suala la ajira kwa vijana waishio karibu na maeneo yanayozunguka mradi, Waziri Mkuu amesema kutakuwa na utaratibu utakaowawezesha vijana walio na sifa kupewa nafasi ya kushiriki kwenye usaili na ikibidi watafanyiwa mchujo kwenye maeneo yatakayofikiwa na wengi. Majaliwa amewataka watakaobahatika kupata ajira kuwa waadilifu na wachapakazi ili kulinda heshima ya vijana wa kitanzania na kuwashawishi wajenzi wa mradi kuajiri vijana wengine zaidi.

Waziri Mkuu pia amezitaka wizara zote zinazoguswa na maandalizi ya ujenzi wa miundombinu inayohitajika katika ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kila wizara inatimiza majukumu iliyopangiwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter