Home KILIMO Usimamizi na utekelezaji wa sheria msingi wa mafanikio ya ushirika

Usimamizi na utekelezaji wa sheria msingi wa mafanikio ya ushirika

0 comment 116 views

Na Ismail Ngayonga,MAELEZO

DAR ES SALAAM

USHIRIKA ni sekta mtambuka inayohusisha sekta mbalimbali zikiwemo Kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Madini, Viwanda, Nyumba na Fedha (Ushirika wa Akiba na Mikopo na Benki) ambazo zinagusa wananchi  wengi zaidi.

Kutokana na umuhimu wa Sekta hii, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imeendelea kuwezesha na kuimarisha Ushirika ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na fursa zinazopatikana na hivyo kuchangia katika kuongeza kipato kwa wananchi wengi hususan waliopo vijijini.

Wizara ya Kilimo inatekeleza malengo yake kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) inayolenga kuleta mageuzi (transformation) ya kilimo kutoka mtazamo uliopo wa kilimo cha kujikimu kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa kibiashara.

Aidha malengo mengine ya programu hiyo ni kuongeza uzalishaji na tija, uongezaji wa thamani wa mazao, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, masoko kwa ajili ya mazao na bidhaa za kilimo na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo huduma za utafiti, mafunzo na ugani.

Serikali na wadau waliamua kuunda sera na sheria mpya kwa ajili ya maendeleo ya ushirika kwa sababu Vyama vingi vya ushirika havijafanikiwa katika uchumi wa soko huru na hivyo kushindwa kutoa huduma za pembejeo, mikopo na masoko ya mazao kwa wanachama.

Kwa mujibu wa Serikali ushirika nchini Tanzania unatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa kanuni za maadili ya kimataifa ikiwemo Elimu, mafunzo na taarifa, Ushiriki wa wanachama katika shughuli za kiuchumi pamoja na Uanachama wa Hiari na ulio wazi.

Kwa nyakati tofauti vyama vikuu vimepoteza mawasiliano na vyama vyao vya msingi na kuanza biashara ambazo hazikuhusiana na zile zilizokuwa zikifanywa na vyama vya msingi, na hivyo mpango uliopo sasa ni kuvifanya vyama vya msingi kuwa ngazi muhimu na ya msingi ya ushirika na kuhakikisha kuwa vyote vinajitegemea na vinadumu.

Akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19, Waziri wa Kilimo,Dkt. Charles Tizeba anasema Wizara ya Kilimo imeendelea kushirikiana na Wizara za kisekta, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wadau wa Maendeleo  kuboresha mifumo ya upatikanaji na usimamizi wa rasilimali, na kujenga na kuimarisha uwezo wa kiuchumi katika Vyama vya Ushirika.

Dkt. Tizeba anasema katika mwaka 2017/2018, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirkiano imefanya uhamasishaji wa wananchi kujiunga au kuanzisha Vyama vya Ushirika ambapo hadi kufikia Desemba 2017 vyama vipya 394 vilisajiliwa na kufanya idadi ya vyama kufikia 10,990 kutoka 10,596 vilivyokuwepo Machi 2017.

“Vyama hivi vinakadiriwa kutoa ajira mpya kwa wananchi takribani1,18 na katika kipindi hicho, wanachama wapya 385,295 walijiunga au kuanzisha Vyama vya Ushirika na kufanya idadi ya  wanachama kuongezeka kutoka 2,234,016 hadi kufikia 2,619,311” anasema Dkt. Tizeba.

Anaongeza kuwa Tume imeendelea kuvijengea na kuimarisha uwezo wa kiuchumi Vyama vya Ushirika wa Akiba na  Mikopo  (SACCOS) ambapo jumla ya Tsh. Bilioni 902 zilitolewa kwa wanachama kama mikopo kwa mwaka 2017 ikilinganishwa na Tsh. Bilioni 855.29 zilizotolewa mwaka 2016.

Kwa mujibu wa Waziri Tizeba anasema SACCOS zimeweza kuongeza akiba na amana za mitaji ya wanachama kufikia akiba ya Tsh Bilioni 561 ikilinganishwa na Tsh Bilioni 331 kwa mwaka 2016 pamoja na kuongeza amana kufikia Tsh. Bilioni  53 kwa mwaka 2017/18 ikilinganishwa na Tsh. Bilioni 47 zilizokuwepo mwaka 2016/2017.

Akifafanua zaidi Dkt. Tizeba anasema katika mwaka 2017/18, Vyama vya Ushirika wa Mazao (AMCOS), vimeendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wakulima ikiwemo huduma za ugani, usambazaji  wa pembejeo, ukusanyaji na uuzaji wa mazao, ambapo Wizara ya Kilimo imeendelea kuwahimiza wakulima kufanya ukusanyaji na uuzaji wa mazao makuu ya biashara kupitia Vyama vya Ushirika.

“Utaratibu huu umesaidia katika kuongeza kiasi cha makusanyo ya mazao kupitia Vyama vya Ushirika, uhakika  wa soko na kuimarika kwa bei za mazao kupitia minada katika mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika mazao mbalimbali yakiwemo pamba, kahawa, ufuta na kakao ili kuwawezesha wakulima kunufaika na bei” anasema Dkt. Tizeba .

Anaongeza kuwa kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, katika msimu wa 2017/18 vyama vya wakulima wa zao la korosho waliuza viliuza korosho na  kuwalipa  wakulima  jumla ya Tsh. Bilioni 1,290.00 ikilinganishwa na malipo ya Tsh. Bilioni 809.18 katika msimu wa 2016/2017.

Ili kufikia malengo ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ni wajibu wa Serikali kuongeza kasi ya ukaguzi wa vyama, kuwajengea uwezo viongozi na kutoa mafunzo kwa wanachama kuhusu haki na wajibu wao kama wamiliki wa vyama.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter