Mkurugenzi wa sensa ya watu na makazi na takwimu za jamii, Ephraim Kwesigabo,amesema mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka unaoishia Oktoba umepungua na kufikia asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.4 kwa mwaka ulioishia Septemba mwaka huu. Kwesigabo ameeleza kuwa, kupungua huko kunamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma imepungua ikilinganishwa na ile ya mwaka ulioishia Septemba.
“Mfumuko wa bei wa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini”. Amefafanua Kwesigabo.
Mkurugenzi huyo amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba umepungua na kufikia asilimia 1.2 kutoka asilimia 2.0 Septemba mwaka huu na kuzitaja baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei wa mwezi Oktoba katika mwaka huu ni pamoja na mchele kwa asilimia 3.8, mahindi kwa asilimia 21.8, unga wa mahindi kwa asilimia 11.6, unga wa mtama kwa asilimia 5.1, unga wa muhogo kwa asilimia 14.1, maharage kwa asilimia 3.0, mihogo mibichi kwa asilimia 5.9, viazi vitamu kwa asilimia 2.1, migimbi kwa asilimia 23.2 na ndizi za kupika kwa asilimia 11.6.
Akizungumzia mfumuko wa bei kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Kwesigabo ameeleza kuwa mfumuko wa bei nchini Kenya kwa mwaka unaoishia Oktoba mwaka huu, umepungua hadi asilimia 5.53 huku nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia Oktoba ukipungua hadi asilimia 3.0 kutoka asilimia 3.7 ya Septemba mwaka huu.