Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. Faustin Kamuzora ametoa wito kwa wakulima wa mpunga katika bonde la Titye wilayani Kasulu mkoani Kigoma kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji yaliyopo sokoni. Katibu huyo ameeleza kuwa serikali imedhamiria kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo kutokana na sekta hiyo kuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025.
“Tumieni fursa zilizowazunguka kwa kuongeza uzalishaji zaidi. Hapa kuna soko la uhakika la bidhaa hii ndani na nje kwani mmezungukwa na soko la nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Lazima tujikite katika uzalishaji wenye tija na unaolenga kumkomboa mkulima kwa kumuongezea kipato chake. Hili linawezekana kwa kuwashirikisha wadau wote muhimu”. Amesema Prof. Kamuzora.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kasulu Simon Anange amesema serikali imeanza kutoa elimu pamoja na kuwahamasisha wakulima kuchukua mikopo benki ili kuongeza uzalishaji wao.
“Tutafanya kila linalowezekana kuwainua wakulima wa zao la mpunga ambalo soko lake ni la uhakika. Tunahimiza pia kilimo bora na chenye tija miongoni mwa wakulima kwa kuwa itaongeza uzalishaji”. Amesisitiza Anange.