Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema serikali imejipanga kuongeza kasi ya malipo ya wakulima wa zao la korosho ili kufikia kiasi cha Sh. 4 Bilioni kwa siku kwani kufanya hivyo kutaharakisha zoezi la malipo. Waziri Hasunga amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Mtwara alipokuwa akitoa tathmini ya hatua zilizofikiwa na serikali katika ununuzi wa korosho za wakulima.
Aidha, Waziri huyo amesema zoezi hilo litaenda sambamba na kuongeza idadi ya wataalamu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya malipo huku akisisitiza kuwa, wataalamu wengine tayari wameshapata uzoefu wa namna ya kuhakiki na namna ya kulipa tangu kuanza kwa zoezi hilo. Ameongeza kuwa mikoa inayolima korosho ni mingi hivyo wakati tathmini pamoja na malipo yakiendelea, timu ya wataalamu wengine itaundwa ili kuanza tathmini mkoani Pwani na mikoa mingine inayozalisha korosho hapa nchini.
Mbali na hayo, Hasunga amesema serikali imejipanga kuwatambua wakulima wote wa korosho nchini ili kuwahudumia kwa urahisi kwani kufanya hivyo kutaimarisha ushirikiano wao na serikali na kuwapa fursa wakulima hao kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo.