Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Susana Mkapa, ameitaka Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB), kuhakikisha inadhibiti maadili ya waajiriwa wa sekta ya ununuzi na ugavi ili fedha za serikali zinazotumika kwenye ununuzi zilete tija kwa watanzania. Mkapa amesema hayo jijini Dodoma, katika hotuba ambayo ilisomwa na Kaimu Naibu Katibu Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Fedha na Mipango, Richard Mkumbo kwa niaba yake, wakati akifunga kongamano la tisa la wataalam wa ununuzi na ugavi kutoka mikoa ya Tanzania bara.
Mkumbo ameeleza kuwa licha ya vitengo vya matumizi mabaya ya fedha za umma kupitia sekta ya ununuzi na ugavi, ikiwemo rushwa kuendelea kupungua, Bodi hiyo inatakiwa kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa na kuongeza kuwa, takribani asilimia 75 ya fedha za umma zinatumika kupitia mchakato wa manunuzi ambao taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mamlaka ya Ununuzi nchini PPRA, umegundua kuwepo kwa mazingira ya rushwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoleta kuleta maendeleo kwa wananchi.
Naye Mwenyekiti wa PSPTB, Sr. Dkt. Hellen Bandiho, amesema Bodi hiyo itahakikisha inasimamia maadili ya watumishi wa sekta ya ununuzi kikamilifu ili kushiriki katika kukuza uchumi.