Home BENKI Benki zashauriwa kushusha riba kuchochea uchumi wa viwanda

Benki zashauriwa kushusha riba kuchochea uchumi wa viwanda

0 comment 41 views

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji ameshauri benki nchini kushusha viwango vya riba za mikopo ili kuwapa nafasi wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na kujiletea maendeleo kutokana na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo. Dk. Kijaji amesema hayo jijini Dodoma wakati anafungua rasmi tawi la benki Azania, Sokoine na kuongeza kuwa, mchango wa benki katika kuisaidia nchi kutimiza azma yake ya kufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji na biashara za wananchi ni mkubwa.

Katika maelezo yake, Naibu Waziri huyo amesema serikali imechukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua, ikiwemo Benki Kuu kutoa mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara na kushusha riba kutoka asilimia 16.0 hadi asilimia 9.0.

“Tumepunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki kuu na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia 17. Kama haya yote yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa kisingizio cha kuogopa mikopo chechefu wakati serikali kupitia Benki kuu, imeanzisha kanzi data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji (Credit Reference Bureau System)”. Amefafanua Dk. Kijaji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe, amesema benki hiyo inaendelea kufanya vizuri katika soko na kwamba, wamejipanga kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter