Home VIWANDAMIUNDOMBINU Kasi ya ujenzi Dodoma yamkera Majaliwa

Kasi ya ujenzi Dodoma yamkera Majaliwa

0 comment 131 views

Baada ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kukagua ujenzi wa eneo la mji wa serikali Ihumwa (Dodoma) na kugundua baadhi ya wakandarasi hawaendi na kasi ya serikali, Waziri huyo ameamua kuitisha kikao cha Mawaziri wote pamoja na Makatibu wakuu ili waeleze kazi hiyo itakamilishwa lini.

“Nimekagua maeneo yote na kukuta baadhi ya wakandarasi wanatakiwa kujenga majengo ya wizara nne hadi tano. Sijaridhika na baadhi ya kazi, nimeitisha kikao cha Mawaziri wote kesho ili tuangalie ni mkandarasi yupi anaweza kumudu hii kazi. Nimebaini kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama kokoto, nondo, matofali na kikao kitahusisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa mkoa na jiji la Dodoma, wakandarasi wote ili tukubaliane kazi hii inaisha lini”. Amesema Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kazi hiyo ina malengo maalum na inapaswa kukamilika haraka kwani tarehe ya mwisho ya kukamilisha ujenzi iliyotolewa na Rais Magufuli ilikuwa Desemba 31.

Pamoja na hayo, Waziri Mkuu amemtaka Mkurugenzi wa jiji la Dodoma, Godwin Kunambi kushirikiana na wenzake na kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata fursa za ajira kwenye mradi huo.

“Mkurugenzi wa jiji wasiliana na Mkurugenzi mwenzako wa Chamwino mhakikishe vijana na akina mama wanakuja kufanya kazi hapa. Pia itisha kikao cha waandishi wa habari uwaeleze wananchi wako fursa zilizopo, kuanzia ufyatuaji wa matofali, uuzaji wa nondo, kokoto na utengenezaji wa pavement blocks, hizi zote ni fursa, tuna wizara 24 na mahitaji ni makubwa”. Amesisitiza Waziri Majaliwa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter