Baada ya kugundua kasoro mbalimbali katika mradi wa maji wa Katoke wilayani Muleba mkoani Kagera, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa onyo kali kwa mkandarasi anayefanya kazi ya ujenzi wa mradi huo wa zaidi ya Sh. 476 milioni baada ya kuwa na kasoro mbalimbali licha ya kukamilika kwake. Aweso amemtaka mkandarasi huyo kuwepo kwenye eneo la mradi na kukagua mradi huo huku akihoji kwanini mradi huo unaonekana kuwa na matatizo, licha ya kwamba umekamilika, unakosa thamani halisi ya fedha.
“Niwaonye watendaji wa Sekta ya Maji, hakikisheni mnawapa kazi wakandarasi wenye uwezo ambao watafanya kazi nzuri na kisha kuidai Serikali malipo yao; sio wakandarasi wajanja ambao wamekuwa wakila fedha za serikali kiholela bila matokeo kuonekana. Ndio maana nimefika Kagera kujionea fedha ambazo Wizara inazitoa kama zinaleta matokeo na sio kuchezewa, huku kilio cha wananchi cha huduma ya majisafi na salama kikiendelea. Jambo hilo halina nafasi kwenye serikali ya awamu ya tano na Wizara ya Maji kwa sasa”. Amesisitiza Naibu Waziri Aweso.