Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua Migahawa ya Kahawa inayotembea ikiwa ni mkakati wa kuongeza ushiriki wa vijana katika mnyororo wa thamani wa Tasnia ya Kahawa nchini.
Majaliwa amezindua migahawa hiyo Agosti 1, 2024 baada ya kufungua Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Nane Nane 2024 yanayofanyika Kitaifa kwenye Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa Wizara ya Kilimo pamoja na Bodi ya Kahawa kwa kufanya ubunifu wa mradi huo ambao utakuwa chachu ya ongezeko la ajira nchini hususan kwa vijana.
Migahawa hiyo ya Kahawa inayotembea, itasimamiwa na Bodi ya Kahawa Tanzania kupitia Mradi wa Jenga Kesho iliyo bora (BBT) ambao upo chini ya Wizara ya Kilimo.