Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amezitaka Bodi zote chini ya Wizara hiyo kuanza usajili wa wakulima wa mazao yote na kuhakikisha wakulima hao wanapatiwa vitambulisho ili waweze kutambulika na kuhudumiwa kwa urahisi. Hasunga amesema hayo wakati akifungua mkutano wa kitaifa wa mwaka wa wadau wa sekta ya Tumbaku Tanzania na kuongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwasaidia wakulima kuboresha kilimo chao na kuweza kupata huduma za uhakika.
“Lazima tuanze kuwatambua wakulima wetu walipo, mashamba wanayolima na ukubwa wake na mazao wanayolima na kiwango mazao ambacho wanatarajia kuzalisha”. Amesema Waziri huyo.
Katika maelezo yake, Waziri huyo ameeleza kuwa, kukosekana kwa takwimu halisi za wakulima, ukubwa wa mashamba yao pamoja na mahali walipo ni changamoto kwa serikali kwani wanashindwa kuwafikishia huduma muhimu kwa ajili ya kuboresha kilimo.
Pamoja na hayo, Waziri Hasunga ametoa wito kwa Bodi ya Tumbaku nchini na wadau wa zao hilo kwa ujumla kuhakikisha wanasaidia kuinua kilimo cha tumbaku ambacho husaidia kuingiza fedha nyingi za kigeni. Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku Tanzania Hassan Wakasuvi amesema moja ya mambo ambayo yanaweza kuinua sekta ya tumbaku ni marekebisho ya Sheria ya zao hilo.