Wizara ya Fedha na Mipango imetoa ruzuku ya Sh. 137 bilioni kwa Halmashauri 12 nchini ili kutekeleza miradi 15 ya kimkakati, itakayowezesha Halmashauri hizo kuongeza mapato ya ndani na kupunguza utegemezi wa kibajeti kutoka serikali kuu. Hafla ya uwekaji wa saini kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa serikali, Dotto James na Wakurugenzi wa Halmashauri imefanyika Jijini Dodoma na kushuhudiwa na Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Dk. Doroth Gwajina pamoja na baadhi ya makatibu tawala wa mikoa ambayo Halmashauri zimepatiwa ruzuku hiyo.
Katibu Mkuu ametoa wito kwa Halmashauri zilizopata fedha hizo kuzitumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, na kutoa onyo kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokiuka makubaliano.
“Maafisa Masuuli mhakikishe mnafuata na kuzingatia Sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 na kanuni zake, ambayo pamoja na mambo mengine inasisitiza juu ya matumizi bora ya fedha kwa shughuli zilizoidhinishwa”. Amesisitiza.
Kwa upande wake, Dk. Gwajima kutoka TAMISEMI ameipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa upatikanaji wa fedha ambazo amesema zitachochea miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini na kuzitaka Halmashauri zilizosaini mikataba kuzingatia malengo na kutekeleza miradi kwa muda na katika viwango vinavyokubalika.