Naibu Waziri wa Kilimo Omary Mgumba amewaambia wabunge jijini Dodoma kuwa, serikali haijanunua kahawa kutoka kwa wakulima kama walivyofanya katika zao la korosho. Mgumba amesema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa kuteuliwa (Chama cha Mapinduzi) Abdallah Bulembo ambaye alihoji:
“Wakulima wana shida, kahawa yao iko katika maghala hawajalipwa hadi leo. Kwanini serikali isifanye kama ilivyofanya katika korosho?”
Katika maelezo yake, Naibu Waziri Mgumba amesema serikali haijanunua kahawa ya wakulima na badala yake, wakulima wenyewe waliamua kuuza kahawa yao mnadani Moshi kupitia vyama vyao vya ushirika. Mgumba amesema kuwa kutokana na kuyumba kwa soko la dunia na kuongezeka kwa uzalishaji bei ya zao hilo imepungua.