Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa ametoa wito kwa wahandisi wote hapa nchini kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu wakandarasi wanaojenga miradi ya maji. Prof. Mbarawa amesema hayo wakati akikagua miradi ya maji inayotekelezwa katika Halmashauri ya wilaya ya Manyoni, ambapo kwa sasa, mradi mkubwa wa maji wa Kintinku/Lusilile awamu ya kwanza unatekelezwa. Mradi huo unatarajiwa kuhudumia wakazi takribani 55,485 kutoka vijiji 11 pindi utakapokamilika na utagharimu Sh. 10,171,877,293.05.
Kwa upande wake, Mbunge wa Manyoni, Daniel Mtuka amemueleza Waziri Mbarawa kuhusu kuanzishwa kwa Mamlaka ya Maji Maua (Maua Water Supply) ambapo Waziri huyo amesema hana pingamizi na kuagizwa wapeleke majina ambayo yatapitiwa na kisha kupitishwa. Prof. Mbarawa amesisitiza kuchaguliwa kwa watu wenye uwezo na sio vinginevyo.
Mbali na hayo, Waziri Mbarawa ameagiza Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) kukamilisha miradi ya kuchimba visima haraka iwezekanavyo na kusisitiza wabadilike kutokana na kutoridhishwa na utendaji wao.