Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba amewataka mawakala waliosambaza pembejeo zikiwemo mbegu na mbolea msimu wa 2015/2016 kuwa wavumilivu kwani vyombo vya uchunguzi vipo mbioni kuhitimisha zoezi hilo. Mgumba amesema hayo kwenye kongamano la tano la wadau wa sekta ya kilimo, mifugo pamoja na uvivu na kueleza kuwa walifikisha suala hilo kwa taasisi za uchunguzi baada ya kugundua tofauti katika deni linalodaiwa na mawakala hao.
“Uchunguzi utakapokamilika, taarifa itatolewa. Jambo hili baada ya serikali ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, kama mnavyofahamu mwaka ukipita wa fedha madeni yote yanahamia Wizara ya Fedha, baada ya kuyachunguza madeni, tukakuta yana ukakasi kidogo, la kwanza bajeti iliyopitishwa mwaka ule ilikuwa Sh. 35 bilioni kwa ajili ya pembejeo zote nchini, lakini vocha zilizotengenezwa zilikuwa zaidi ya Sh. 70 bilioni, ukakasi wa kwanza huo” Amesema Mgumba na kuongeza:
“Kutokana na hali hiyo, tukaona tujiridhishe, tufanye uhakiki wa kina tuone tatizo ni nani waliotengeneza na kujinufaisha, uchunguzi huo umefanyika na kila aina ya kila aina ya uchunguzi unaoujua wewe, na taarifa tulizokuwa nazo za awali kuna hujuma kubwa iliyofanyika kwa namna moja au nyingine wapo watumishi wa serikali, mawakala wenyewe na viongozi huko chini”. Amesema Naibu huyo.