Meneja Mwandamizi wa Mipango na Utafiti wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) John Fwalo, amewataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa ya kuuza kahawa na viungo nchini Ukraine ili waweze kuendeleza biashara zao na kukuza pato la taifa. Meneja huyo amesema kuwa mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na Ukraine yamekuwa yakiendelea kwa kasi, jambo ambalo limewapa upenyo wajasiliamali nchini kufanya biashara. Pia ameeleza kuwa majadiliano baina ya nchi hizo yanalenga kuweka sera ambazo zitawafaidisha watanzania hasa katika masuala ya biashara nchini Ukraine.
“Tupo hapa kuzungumza na kuwahamasisha watanzania kufanya biashara zao na Ukraine hususani katika kahawa, viungo na bidhaa nyingine za viwandani. Fursa hii itasaidia kupanua wigo wa biashara zao na kuongeza thamani ya soko la Ukraine kwa watanzania”. Amesema Fwalo.
Pia amesisitiza kuwa fursa hiyo ni muhimu sana kwa wafanyabiashara wa kahawa kwani nafasi hiyo itaongeza mapato kwa wafanyabiashara hao na hivyo kuwataka kufuata vigezo ili waweze kufanya biashara nchini humo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Usindikaji wa Chakula mbalimbali nchini (TAFOPA) Suzy Laizer amesema kuwa huu ni muda muafaka kwa wafanyabiashara nchini kujiunga kwa pamoja ili kushughulikia fursa ipsavyo fursa iliyopo Ukraine.