Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof. Simon Msanjila amesema Wizara hiyo ipo mbioni kukamilisha taratibu za kutoa leseni kwa migodi mikubwa. Prof. Msanjila mesema hayo wakati wa mkutano wake na viongozi wa Jumuiya ya Watendaji Wakuu wa Taasisi Binafsi na kusema kuwa, leseni hizo hazijawahi kutolewa nchini na kwamba migodi hiyo inatarajiwa kuanzishwa hivi karibuni.
Viongozi hao walikutana na Katibu huyo kwa lengo la kujitambulisha na vilevile kuelewa sekta ya madini, mabadiliko ya Sheria ya Madini na namna wanavyoweza kushirikiana ili kuendeleza sekta husika.
Akieleza kuhusu Sheria Mpya ya Madini ya Mwaka 2017, Prof. Msanjila amesema hakuna tatizo katika utekelezaji wa Sheria na Wizara hiyo inapokea wawekezaji wengi wenye nia ya kuwekeza nchini bila kikwazo.
“Hakuna mahali ambapo serikali inatengeneza Sheria kwa ajili ya kumkandamiza mfanyabiashara. Hakuna tatizo lolote kwenye Sheria ya Madini. Hata wageni huwa tunakaa nao tunawaelimisha na wanatuelewa vizuri. Kama kuna dosari ni vitu ambavyo tunaweza kuvirekebisha na tayari tumekwisha kufanya hivyo kwa baadhi ya maeneo”. Amesema Prof. Msanjila.