Wakulima wa kata ya Pangwi wilaya ya Kilindi mkoani Tanga wamepata hasara kufuatia ekari zaidi ya 2000 kushambuliwa na viwavijeshi. Ofisa Kilimo wa Kata hiyo, Dustan Emmanuel ametoa uthibitisho kuhusu janga hilo huku akitaja kijiji cha Nyamaleni kuathirika zaidi na janga hilo.
Alex Mhando, mmoja wa wakulima ameeleza kuwa shambulio la wadudu hao limewaathiri sana hasa kwa kuwa wakulima hao wanategemea kilimo ili waweze kujikimu kimaisha. Mkulima mwingine, Cosmas Chingwaba ametoa wito kwa au serikali kuwasaidia pale itakapotokea wanahitaji chakula kwani uharibifu wa mazao yao utaleta janga la njaa kati ya wakulima hao.
Ofisa Kilimo huyo amewaondoa hofu wakulima waliopo karibu na kata hiyo kwani hadi sasa tatizo hilo linashughulikiwa ipasavyo na wataalamu ili kupata suluhisho na kuzuia lisiendelee kusambaa katika maeneo mengine. Aidha, Kituo cha Kuthibiti Magonjwa ya Mimea cha Tengeru Mkoani Arusha, kimeanza kutoa elimu kwa wakulima hao ili wajue jinsi ya kukabiliana na hali kama hiypindi inapotokea .