Makamu wa Rais wa Tanzania. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwa wakulima mkoani Shinyanga kwa kuzalisha kwa wingi mazao ya biashara na chakula na kufanya mkoa huo kujitosheleza kwa akiba ya chakula tofauti na mikoa mingine. Makamu huyo amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wilayani Kahama na kueleza kuwa, katika msimu uliopita, Shinyanga ilizalisha zaidi ya tani 500,000 za mazao ya biashara na chakula.
Aidha, Samia amewataka wakulima hao kuendeleza jitihada na kulima kwa wingi huku akiwasisitiza kuuza nchi za jirani kwani sekta ya kilimo huingiza fedha za kigeni kwa wingi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa amesema kufuatia uzalishaji wa mazao ya biashara kuwa wa juu, serikali imepanga kuanzisha kiwanda kikubwa cha usindikaji wa mazao Kanda ya Ziwa ili kurahisisha nchi jirani kama Rwanda, Burundi, Congo na Uganda kufanya manunuzi.
Pamoja na hayo, Naibu huyo ameeleza kuwa serikali imekuwa ikipeleka pembejeo kwa wakulima kwa wakati na vilevile kuwatafutia soko ili kuwawezesha wakulima hao kujiongezea kipato.