Baada ya mafuta ya petroli kulipuka na kusababisha ajali ya moto katika kijiji cha Marwa, Same mkoa wa Kilimanjaro, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) ipo katika harakati za kurekebisha kanuni zinazoelekeza ujenzi wa vituo vya mafuta vijijini.
Meneja Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo amethibitisha hilo na kueleza kuwa tayari wamesharekebisha kanuni ya ujenzi ambayo inamtaka muwekezaji kuwekeza Shilingi milioni 400 hadi bilioni moja, tofauti na sasa ambapo muwekezaji anaweza kuwekeza hadi kwa Shilingi milioni 50.
“Kwa kupunguza masharti ya gharama za ujenzi watu wengi watawekeza vijijini. Lakini la pili ni kwamba Ewura imemtafuta mtaalamu mwelekezi ili kutengeneza vituo vya kutembea (mobile)”. Amesema Kaguo na kuongeza:
“Mfumo unaopendekezwa utakuwa ni tenki dogo la mafuta kuwekwa kwenye vigari vidogo kama kirikuu au pikipiki ya magurudumu matatu, ambazo zitajaza mafuta sema lita 100 au 50”.
Meneja huyo amewataka wananchi kuwa makini na biashara holela ya mafuta madukani na kueleza kuwa mfumo huo mpya bado upo kwenye hatua za awali hivyo kuwataka wananchi kuwa wavumilivu.