Mtaalamu Michael Malembeka kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ametoa wito kwa vijana kujituma na kutumia fursa mbalimbali katika jamii kujiletea maendeleo badala ya kukumbatia umaskini. Malembeka amesema hayo wakati wa mafunzo ya kutengeneza na kusindika bidhaa mbalimbali Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaam.
“Kwenye maisha kuna vitu viwili, utajiri na umaskini. Kijana unaweza kuamua kuzingatia mafunzo haya au kuyaacha na usitegemee mtu katika maisha yako, lakini ukumbuke umaskini una sifa kuu mbili. Hivyo msiuvumilie….utasikia mtu anasema mimi ni maskini nitafanyaje, hapa ina maana unauvumilia umaskini, vijana jitumeni kwa kupambana kwa dhati na adui huyu ili kuhakikisha mnafanikiwa katika maisha yenu”. Ameeleza Mtaalamu huyo.
Naye mmoja wa viongozi kutoka taasisi inayoratibu mafunzo hayo, Mpakani Tunaweza, Hussein Wamaywa amewataka vijana kujifunza kitu kutoka kwenye mafunzo hayo na kujiendeleza.
“Mnafundishwa kutengeneza vitu vingi, na inawezekana kijana usipendelee kitu fulani, lakini ni muhimu upeleke ujuzi huo katika jukwaa lako, mwenzako anaweza kupenda ujuzi wa kile ambacho wewe hupendi”. Amesema Wamaywa.