Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi mkoani Singida, Justice Kijazi amesema kuanzia Julai mwaka 2018 hadi sasa, Halmashauri hiyo imetoa mikopo ya takribani Sh. 85.9 milioni kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwainua kiuchumi.
Fedha hizo zimesaidia vikundi hivyo kuendeleza shughuli zao za kimaendeleo na kuchangia pato la taifa. Katika maelezo yake, Kijazi amesema kuwa, mikopo hiyo imeelekezwa kwenye vikundi kutoka vijiji mbalimbali ambavyo vinafanya shughuli za ufugaji, ujasiriamali, biashara pamoja na kuweka na kutoa fedha.
“Mikopo tunayowapa haina riba na inatolewa kwa mwaka mmoja, vikundi vinavyopata mikopo mikubwa vinapewa muda wa miezi mitatu wa kujipanga, wastani wa watu kwenye vikundi ni kuanzia saba isipokuwa vikundi vya Vicoba vyenye watu 30”. Ameeleza Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Haika Massawe amesema changamoto iliyopo ni uhitaji mkubwa wa mikopo kulinganishwa na fedha inayotolewa, marejesho kutofanywa kwa muda uliopangwa hususani kwa vijana na baadhi ya vikundi kukosa miradi endelevu.
“Mikopo imesaidia wanavikundi kugharamia huduma za kijamii kama afya na mahitaji ya shule kwa watoto wao”. Amesema.