Kaimu Katibu Tawala mkoani Dodoma, Happiness Mgalula amewashauri wakulima wa zao la alizeti kutumia mbinu za asili kuzalisha zao hilo ili waweze kukidhi vigezo vya soko la kimataifa hususani nchini Ulaya na India.
“Alizeti ni miongoni mwa mazao yaliyopewa kipaumbele kuzalishwa hapa nchini kutokana na umuhimu wake katika kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula ndani na nje ya nchi hivyo tutumie mbinu za asili katika kuzalisha zao hili”. Amesema Mgalula.
Katika maelezo yake, Mgalula amesema zao hilo linachangia asilimia 51 ya mafuta yote yanayozalishwa na kuwataka wakulima kutumia njia za asili kama mbolea kupanda mbegu bora pamoja na kutumia viuatilifu vinavyoshauriwa na wataalamu wa kilimo katika eneo husika ili kuongeza uzalishaji.
Mkoa huo tayari una viwanda 432, kati ya hivyo viwanda vikubwa vinavyosindika alizeti ni 6, vya kati 19 na viwanda vidogo ni 407. Aidha, Mgalula ameeleza kuwa mahitaji ya mafuta hapa nchini yanaendelea kuongezeka na yanakadiriwa kuwa ni mita za ujazo 300,000 hadi mita 400,000.