Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa wizara hiyo ina mpango wa kuingiza kwenye gridi ya taifa umeme megawati 10,000 hadi kufika mwaka 2025 kutoka megawati 1,602 ya sasa. Mgalu amesema hayo bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainab Katimba aliyeuliza kuhusu mkakati ambao serikali wameweka ili kuweza kuzalisha megawati 5,000 za umeme hadi mwaka 2020.
Naibu Waziri Mgalu amesema serikali imejipanga kutumia vyanzo mbalimbali vya maji, gesi na jua ili kutekeleza azma hiyo.
“Miongoni mwa miradi hiyo ni wa upanuzi wa miradi wa kufua umeme kutumia gesi asilia ya Kinyerezi I kutoka megawati 150 hadi megawati 335 ambao utakamilika Agosti 2019”. Amesema.
Pia ametaja miradi ya kufua umeme kuwa ni Kinyerezi II wa megawati 240 mradi huu ulikamilika April mwaka jana, mradi wa megawati 300 ambao upo chini ya ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Japan (JICA) ambao unategemea kuanza rasmi machi 2020, mwingine ni wa Ruhuji wa megawati 358, mradi wa Rumakali megawati 222, Kakono megawati 87 ambayo itakamilika mwaka 2021.
“Desemba 2018, serikali ilianza kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji wa megawati 2,115 pamoja na miradi wa umeme wa Rusumo megawati 80”. Amefafanua Naibu Waziri huyo.