Home FEDHA Sababu mishahara kutopanda yatajwa

Sababu mishahara kutopanda yatajwa

0 comment 102 views

Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa watumishi wa umma kuwa wavumilivu wakati huu ambao azma kubwa ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuahidi kutoa nyongeza ya mishahara kabla ya kutoka kwenye kiti cha urais. Rais Magufuli ametoa ahadi hiyo mkoani Mbeya wakati wa maadhimisho ya kitaifa ya Mei Mosi yaliyokuwa na kaulimbiu ‘Tanzania ya uchumi wa viwanda inawezekana, wakati wa mishahara na maslahi bora ni sasa’.

Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika viwanja vya Sokoine, Rais amefafanua kuwa mishahara ya watumishi haijaongezeka kwa sababu kufanya hivyo kungepelekea bei za bidhaa mbalimbali sokoni kupanda.

“Ni kweli nilitoa ahadi hiyo ya nyongeza ya mishahara lakini ni lazima tuelewe hadi sasa sijaondoka madarakani, naomba muamini subira yavuta heri ningeweza kupandisha ila muda wangu bado haujaisha, ningeweza kutamka napandisha mishahara nikaongeza Sh. 5,000 au 10,000 kwenye mishahara yenu, ningetamka hivyo kesho bidhaa zingeanza kupanda, mafuta ya taa yangepanda, ukitaka mahindi yangepanda, usafiri ungepanda lazima tujenge uchumi imara”. Amesema Rais Magufuli na kuongeza:

“Bado ndugu zangu sijaondoka madarakani kwa maelezo niliyoyaeleza yanaonyesha uchumi wetu unakwenda vizuri kwenye uchumi wa kati, hatua tulizochukua na tunazoendelea kuchukua zinawanufaisha wafanyakazi na watanzania wote. Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa asilimia za juu, kwa miradi inayotekelezwa na uchapakazi wa wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, tunaelekea pazuri. Nimeamua kuwaeleza ukweli, kwa sababu ukweli utabaki kuwa kweli, wafanyakazi tuvumilie, sikutaka niwapake uji kwa kutamka hapa nimepandisha mishahara halafu mkute hazipo, lazima tujipange vizuri na nafikiri tupo kwenye muelekeo mzuri, nitaboresha maslahi kulingana na uwezo wa serikali”. Ameeleza JPM.

Kuhusu ombi watumishi walio na elimu ya darasa la saba ambalo lilitolewa na Shirikisho Huru la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Rais Magufuli amesisitiza kuwa serikali haina ubaguzi na kwamba kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wafanyakazi takribani 98, 615 kati ya 525,509 wana elimu hiyo.

“Mmeomba kuhusu usalama kwenye sehemu za kazi na vyama vya wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi, waajiri toeni mikataba ya ajira, mruhusu hivi vyama maeneo yenu, mamlaka hakikisheni Sheria hizi zinafuatwa”. Amesema Rais.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter