Home BIASHARA Jinsi ya kufanya usajili wa BRELA mtandaoni

Jinsi ya kufanya usajili wa BRELA mtandaoni

0 comment 320 views

BRELA ni wakala wa serikali ulio na mamlaka ya usajili wa kampuni na majina ya biashara. Zamani wamiliki wa kampuni au biashara walikuwa wanatakiwa kufika katika ofisi za BRELA kwa ajili ya kujisajili kupitia mfumo wa awali uliokuwa ukijulikana kama OBRS, jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kwa sababu ilikuwa inawabidi kusubiri kwa muda mrefu ili kukamilisha mchakato mzima.

Mwaka jana, BRELA walitangaza kufunga rasmi mfumo wa OBRS na kuanzisha mfumo mpya wa ORS ambao unamuwezesha mmiliki na mfanyabiashara kusajili jina la kampuni au biashara mtandaoni kwa kupitia tovuti yao badala ya kufika katika ofisi za taasisi hiyo.

Kwanza kabisa, kama hauna akaunti kwenye tovuti ya BRELA unatakiwa kutengeneza akaunti katika tovuti hiyo. Nenda https://ors.brela.go.tz/um/register kwa ajili ya kutengeneza akaunti hiyo.

Hizi ni hatua za kufuata ili kujisajili:

TAARIFA ZA MSAJILI

Ili kujisajili unatakiwa kuwa na taarifa zifuatazo

  • Kitambulisho cha taifa kwa mtanzania (kinatolewa na NIDA) na Passport kwa raia wa kigeni
  • Namba ya simu ya mkononi
  • Barua pepe

TAARIFA ZA KAMPUNI/BIASHARA

Hapa unahitaji kuwa na mambo yafuatayo,

  • Jina la kampuni
  • Aina ya kampuni
  • TIN namba
  • Tarehe ya kufunga mahesabu

TAARIFA KUHUSU ENEO LA KAMPUNI/BIASHARA

Hapa inahitajika kueleza eneo ofisi yako itakapokuwa inapatikana

  • Aina ya eneo (kama limepimwa au la) kama halijapimwa hakikisha una anuani ya makazi kama ifuatavyo: jina la mkoa, wilaya, kata, kijiji, kitongoji na ueleze kama eneo lipo karibu na alama zipi ambazo hazihamishiki kama shule ya msingi n.k. Usiweke alama ambazo hazina uhakika wa kudumu
  • Kama eneo limepimwa basi weka vielelezo hivi : jina la mkoa, wilaya, kata, kijiji/mtaa, barabara, namba ya kiwanja, kitalu na nyumba, sanduku la posta, simu ya ofisini au kiganjani na barua pepe..

Baada ya kuweka taarifa hizo, elezea shughuli za kampuni au biashara hiyo.

TAARIFA ZA WAKURUGENZI

Baada ya kueleza kuhusu shughuli za kampuni/biashara unatakiwa kuwa na taarifa kuhusu wakurugenzi wa kampuni au biashara husika kama ifuatavyo:

  • Aina ya Mkurugenzi, kama ni mtu binafsi au ni taasisi
  • Kama ni mtanzania au mgeni
  • Kitambulisho cha taifa au passport
  • TIN
  • Namba ya simu
  • Barua pepe
  • Anuani za makazi ya Mkurugenzi : Kama eneo limepimwa basi weka vielelezo hivi : jina la mkoa, wilaya, kata, kijiji/mtaa, barabara, namba ya kiwanja, kitalu na nyumba, sanduku la posta, simu ya ofisini au kiganjani na barua pepe.
  • Kama halijapimwa hakikisha una anuani ya makazi kama ifuatavyo : jina la mkoa, wilaya, kata, kijiji, kitongoji na ueleze kama eneo lipo karibu na alama zipi ambazo hazihamishiki. Usiweke alama ambazo hazina uhakika wa kudumu.

TAARIFA ZA KATIBU WA KAMPUNI

Hapa taarifa zinazohitajika ni kama zile za Mkurugenzi, tofauti yake ni mhusika tu. Hivyo maelezo ya kufuata ni kama hayo yaliyoainishwa kuhusu taarifa ya Mkurugenzi.

TAARIFA ZA MWANACHAMA/WAMILIKI WA HISA

Hapa pia taarifa zinazohitajika ni kama zile za Mkurugenzi.

VIAMBATANISHO

Hapa mtu au taasisi inayojisajili hutakiwa kuambatanisha taarifa zifuatazo:

  • Memorandum and articles of association(https://www.kivuyo.com/jinsi-ya-kuandika-memart-memorundum-and-article-of-association/) iliyosainiwa na wanachama/wenye hisa pamoja na mwanasheria wa umma.
  • Fomu ya 14b iliyosainiwa na mmoja wa wakurugenzi na mwanasheria wa umma (Notary Public)
  • Pamoja na fomu ya Maadili na uadilifu (Ethics and Integrity) iliyosainiwa na mmoja wa wakurugenzi.
  • Fomu ya kuimarisha kampuni au biashara (Company consolidated form) iliyosainiwa wakurugenzi wote na katibu wa kampuni.

NJIA YA MALIPO

Hapa kuna njia mbili ambazo ni:

  • Kulipa kwa kuweka fedha kwenye akaunti ya benki kupitia namba ya kumbukumbu ambayo utapata kupitia PO yako
  • Kwa njia ya simu ya mkononi kupitia mitandao ya simu. Unatakiwa kuweka namba ya kampuni ambayo ni 888999 na kumbukumbu ya malipo uliyopewa kupitia PO yako.

Ili kufikia hatua hii ya mwisho, unatakiwa kujaza hatua zote za mwanzo. Ifahamike kuwa unaweza kujisajili kwa muda wa siku sita, kama hujamaliza kujaza taarifa baada ya siku sita basi taarifa ulizofanikiwa kuzijaza zitafutwa, hivyo utalazimika kujaza taarifa zote upya.

Ni muhimu kusajili jina la kampuni au biashara yako ili kuepukana na usumbufu.

 

 

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter