Mkataba ni muhimu kwa muajiri na muajiriwa, hasa kwa sababu husaidia pande zote mbili kupata wanachotaka nikimaanisha muajiri kuhakikisha shughuli zake zinaenda vizuri na maendeleo katika kampuni/ofisi yake yanaonekana na kwa upande wa muajiriwa, anafurahi kufanya kazi katika kampuni/ofisi ya muajiri bila adha yoyote kwa mfano kucheleweshewa mshahara, mazingira mabovu kazini n.k.
Ni muhimu kufanya mikataba ya maandishi kuliko kufanya mikataba ya maneno kwani inakuwa rahisi kufanya maamuzi kwa muajiri na muajiriwa kutokana na uwepo wa nyaraka zinazoweza kuwa muongozo sahihi.
Muajiri na muajiriwa wakiandikishana mkataba kwa njia ya maandishi inakuwa rahisi kwa pande zote mbili kufanya kazi vizuri na kukidhi matakwa na malengo ya kampuni ikiwa ni pamoja na muajiri kujua majukumu yake na muajiriwa pia kutekeleza majukumu yake ili hali akitambua changamoto atakayoweza kuzipata kama hatotimiza majukumu yake kama ilivyoandikwa katika mkataba.
Kila ofisi au kampuni siku zote hutaka kupata maendeleo, kupitia mkataba hilo linaweza kuchochea kampuni au ofisi husika kujipatia mafanikio kwa kuwa kila mtu (muajiri na muajiriwa) atajituma na kushirikiana kuleta mafanikio katika kampuni kwa kufuata kanuni na sheria zilizoandikwa katika mkataba.
Kupitia mikataba, siri za kampuni au ofisi huwa ni vigumu kutoka nje ya ofisi na kuwafikia washindani katika tasnia husika, na hii ni kwa pande zote mbili muajiriwa na muajiri. Ikitokea mmoja kati yao amekiuka hilo, basi muajiri au muajiriwa huruhusiwa kuchukua hatua za kisheria.
Kuhusu mapumziko au likizo, ruhusa na mambo yanayoendana na hayo muajiri na muajiriwa huwekeana maelezo katika mkataba ili kuepusha sababu zisizokuwa na msingi zinazoweza kutokea mara kwa mara hasa katika upande wa muajiriwa. Kwa mfano, ikitokea muajiri na muajiriwa wamesaini mkataba inakuwa rahisi kwa muajiri kujua haki za mtu aliyemuajiri na nini kifanyike iwapo mfanyakazi wake anaomba sana ruhusa na ni kiasi gani inaleta shida kwa ofisi.
Ni muhimu kwa muajiri kumkumbusha muajiriwa mara kwa mara mambo ya kuzingatia hususani yaliyopo katika mkataba ili kuepukana na hatua mbadala ambazo zinaweza kuumiza pande zote mbili.
Aidha, muajiriwa anashauriwa kusoma kwa makini mkataba kabla hajausaini ili kuepuka shida yoyote huko mbele kama atahitajika kufanya mambo ambayo yapo nje ya uwezo wake. Lengo la mkataba siku zote huwa ni kuhakikisha pande zote mbili zinafurahia kufanya kazi pamoja na si vinginevyo.