Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kwa mwaka wa masomo 2017/2018 wanafunzi zaidi ya 30,000 watapata mikopo kulingana na fani walizochagua kujiunga nazo vyuoni.
Bodi ya mikopo imepanga kutoa mikopo hiyo kwa mikondo mitatu. Mkondo wa kwanza utawanufaisha wanafunzi wa masomo ya afya, sayansi ya elimu na hesabu ambapo watapata asilimia 40 ya bajeti ya fedha zilizotengwa kwa mikopo yote.
Mkondo wa pili utapata asilimia 35 ya mkopo na itahusisha wanafunzi wa masomo ya uhandisi, misitu, kilimo, usafirishaji na sayansi ya ardhi huku mkondo wa tatu ukipokea asilimia 25 na watakaonufaika ni wanafunzi wa masomo ya sanaa, lugha, jamii na fani zinazofanana na hizo.
Badru amesema kuwa wanafunzi wa masomo ya sayansi watapata mikopo mikubwa kuliko wengine kwa sababu fani hizo ni adimu na zina mahitaji makubwa kisoko kuliko makundi mengine. Mbali na kutoa mikopo hiyo kwa kuangalia masomo ya wanafunzi pia bodi ya mikopo itaangalia jinsia na kuhakikisha jinsia zote zinapata mikopo hiyo kwa usawa.