Na Mwandishi wetu
Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA PHASE III) umezinduliwa katika kijiji cha Kabwe wilayani Nkasi mkoa wa Ruvuma. Akiwa kwenye uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema mradi huo utagharimu jumla ya Sh 42.5 bilioni na utatekelezwa katika vipindi viwili tofauti.
Awamu ya kwanza ya mradi huo utapeleka umeme kwa vijiji 111 huku awamu ya pili ambayo itaanza punde tu baada ya awamu ya kwanza kumalizika, itahusisha vijiji 145. Mpaka kufikia mwaka 2012 vijiji vyote katika mkoa wa Rukwa vitakuwa vimepelekewa umeme kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Kwenye uzinduzi huo Naibu Waziri pia alimtambulisha mkandarasi atakayejenga mradi huo ambaye ni Nakuroi Investment Company Limited ya hapa nchini. Mkandarasi huyo ametakiwa kuhakikisha kuwa kila kijiji na kitongoji kinapelekewa umeme. Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) nalo limetakiwa kufungua ofisi katika kijiji cha Kabwe na katika maeneo yote yaliyo na wateja wengi ambao wapo mbali na huduma za shirika hilo.
Wananchi wa kabwe nao wameshauriwa kuwa waamifu na kushirikiana na TANESCO kabla na baada ya kumalizika kwa mradi huo. Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy naye ameomba wananchi kushirikiana na mkandarasi, na pia kuwakumbusha kuwa mradi huo wa umeme kijijini hapo hautakuwa na malipo ya fidia.