Kiasi cha fedha unachotumia kulipa kodi ya nyumba kinaweza kukuletea changamoto za muda mrefu. Sawa kila mtu akiwa anatafuta sehemu ya kukaa hujitahidi kutafuta sehemu ambayo ana uwezo wa kulipia lakini hiyo haimaanishi kuwa fedha zako nyingi uzielekeze katika kodi kwani kwa kufanya hivyo mambo yako mengine yanayohitaji fedha yatasimama au kuathirika kwa namna moja au nyingine kutokana na fedha zote kuelekezwa sehemu moja.
Hivyo hizi ni njia mbalimbali za kupunguza kiasi cha fedha unachotumia kulipa kodi ya nyumba
ENEO
Hapa unatakiwa kutafuta eneo ambalo ni la wastani, nikimaanisha kuwa hulipi kodi kubwa sana na hutumii fedha nyingi kufika kazini au hutumii fedha nyingi katika matumizi ya kila siku na vitu unavyotamani. Hivyo tafuta seheme yenye usafiri wa rahisi, na kodi unayoweza kumudu ili kuhakikisha mambo yanaenda na hutumii fedha nje ya bajeti yako.
MAMBO MAZURI
Badala ya kutafuta sehemu nzuri ya bei ghali, angalia kipato chako na tafakari kama maamuzi hayo ni sahihi. Pia usitafute sehemu ambayo inahitaji marekebisho makubwa kwa sababu hii itaharibu bajeti yako, hivyo tafuta sehemu ambayo inaridhishwa isiyohitaji marekebisho mengi na yenye kodi inayoendana na kipato chako. Usiishi kwa kuwafurahisha watu.
MTU/WATU WENGINE
Unaweza kubana matumizi na kupata sehemu nzuri ikiwa unaweza kukaa na watu wengine. Watu wengi huamua kufanya maamuzi hayo ili waweze kulipia kodi kubwa katika maeneo mazuri au yaliyopo karibu na kazi. Hivyo tafuta mtu au watu ambao unaamini ukikaa nao hakutakuwa na shida, wekeni mfumo na kanuni ambazo zitawasaidia kuishi vizuri na kwa urahisi.
JUA UNACHOTAKA
Wakati unatafuta sehemu ya kukaa unatakiwa kujua vitu ambavyo unataka viwepo katika nyumba kulingana na bajeti yako. Weka kila kitu tayari ikiwa utaridhishwa na nyumba muda wowote hasa nyumba za bei ya chini kwa sababu kila mtu anapenda vitu vya bei rahisi. Hivyo kuwa na nyaraka zote zinazohitajika kutarahisisha kupata nyumba ya bei rahisi haraka. Pia jitahidi kuomba kupunguziwa nyumba hii ni nzuri kwa upande wako hasa katika sehemu unayoitaka hii itakuwa ni sawa na kushinda vitu viwili kwa muda mmoja.
TAAARIFA MUHIMU
Ni muhimu kujua taarifa zote kuhusu mahali unapoishi ili kuepuka na changamoto zozote mbeleni, hivyo muulize mpangishaji maswali mengi kuhusu eneo husika ili kujua kama utaweza kumudu sehemu hiyo ikiwa pamoja na sheria na masharti yaliyopo. Kwamfano unaweza kuuliza kama kuna matatizo yoyote kuhusu wadudu, kama kuna kelele zinazotokana na miziki,kanisa nk.
Jambo la muhimu zaidi ni kujua ikiwa utabadilisha kazi, hufurahishwi na eneo,nyumba, au unatakiwa kuhamia mkoa, mji, nchi nyingine na kodi yako haijaisha, je utalipwa kiasi cha fedha kilichobaki? Kujua hili kutaepushwa kulipa fedha ya muda mrefu na kufanya maamuzi. Pia unatakiwa kuuliza kama kuna kawaida ya kuongeza kodi kutokana na mwenendo wa fedha.
Hivyo chukua muda, usifanye maamuzi haraka kwa sababu baada ya malipo sehemu hiyo inakuwa ndio nyumbani kwako. Na siku zote nyumbani ni mahali kwa kupumzika, na kuwa na amani na si vinginevyo.