Home BIASHARA Unapopanga bei zingatia haya

Unapopanga bei zingatia haya

0 comment 87 views

Upangaji wa bei ya bidhaa au huduma unaweza kuleta faida au hasara katika biashara. Hivyo ni muhimu kuangalia mambo mbalimbali na kutafakari kwa kina kabla hujafanya maamuzi kuhusu bei ya bidhaa/huduma yako.

Mambo ya kuzingatia:

Gharama

Hili ni jambo la kwanza kuzingatia ni gharama ulizotumia kuanzisha biashara nzima. Hakuna biashara ambayo inaweza kujiendeleza yenyewe kama gharama zinazidi mauzo. Njia rahisi ya kuweza kupanga bei ya bidhaa ni kuchukua gharama ulizotumia na kuongeza asilimia ya kawaida katika gharama hizo. Kwa kufanya hivyo utakuwa na uhakika wa faida ili mradi mauzo yawe yanafanyika. Faida inaweza isiwe kubwa sana lakini itakuwepo. Kwa mfano unauza magauni, umenunua magauni kwa Sh. 2000 hapo unaweza kuongeza Sh. 3000 na kuuza gauni kwa Sh. 5000.

Thamani

Siku zote mteja huwa tayari kulipia kitu ambacho anafikiri kina hadhi ya kuuzwa kwa bei husika. Ikiwa umeweka bei kubwa katika bidhaa ya kawaida basi tambua wateja hawatonunua bidhaa yako. Thamani ya bidhaa huwa katika akili ya mteja hivyo unatakiwa kufikiria je kama ungekuwa mteja ungenunua bidhaa hiyo kwa bei unayoweka? Kwa kujibu hilo itakuwa rahisi kuweka bei ambayo itawavuta wateja na kukuletea faida.

Washindani

Ili kupata faida zaidi kupitia bei utakayoipanga unatakiwa kufikiria tofauti na washindani wako ili kupata wateja wengi zaidi. Sawa kuna bidhaa ambazo zina bei rasmi lakini hiyo isikurudishe nyuma kuwahamasisha wateja wengi kununua zaidi. Unaweza kuuza bidhaa zenye ubora zaidi, au unaweza kuweka biashara yako sehemu ambayo watu wengi hupita au huhitaji bidhaa hizo zaidi katika muda fulani.

Hatari ya kuharibika

Hatari ya bidhaa kuharibika ni moja ya mambo ambayo unatakiwa kuzingatia ikiwa unapanga bei. Kuweka bei juu kwa vitu ambavyo vinaharibika kwa urahisi kutaleta hasara katika biashara yako. Ndio maana mfanyabiashara hushauriwa kupunguza bei kwa vitu ambavyo vinahitajika kwa muda mfupi. Mfano mapambo ya Christmas, vitu vinavyokaribia kuisha muda wa matumizi (expiry date) nk.

Vivutio

Faida ni muhimu katika biashara lakini ni muhimu zaidi kuweka bidhaa ambazo zinawavutia wateja hata kama hazina faida kubwa au faida kabisa. Kwa mfano kwa wateja wa bidhaa za rejareja ni muhimu kuwa na bidhaa kama vocha, ambazo ni muhimu kwa watu wengi na ikiwa mteja amepata vocha ni rahisi kuvutiwa na bidhaa nyingine.

Vilevile ni muhimu kumpa mteja machaguo tofauti kwa mfano badala ya kulipa milioni 2 kwa mwezi mteja anaweza kulipia milioni 1 kila baada ya wiki mbili. Hata kama ni kitu kile kile mteja ataona ni rahisi kwani watu wana majukumu mengi na urahisi wa malipo huvutia watu kutokana na kwamba wanakuwa na uwezo wa kufanya mambo mengi kwa muda mmoja.

Zingatia malengo yako ili kuweza kufanya maamuzi sahihi kuhusu bei ya bidhaa au huduma unayoiuza kwa wateja.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter