Kawaida benki nyingi huweka vigezo na masharti kwa wakopaji kabla hawajapata mkopo. Moja ya masharti ambayo wafanyabiashara wadogo hushindwa kutimiza ni dhamana, kwa sababu wafanyabiashara hao bado hawana mali za kutosha kuwekeza ili kupata mikopo benki na wakati huo huo, wafanyabiashara wengine hawataki kuhatarisha mali zao binafsi kwa sababu ya mkopo.
Hali hii imepelekea taasisi nyingi za fedha mbali na benki kujitokeza na kutoa mikopo katika biashara ndogo bila dhamana. Ieleweke kuwa kutoa mkopo bila dhamana inaweza kuwa ni jambo la hatari hasa kwa mkopeshaji na ndio maana wakopaji bila dhamana hutozwa viwango vikubwa vya riba. Pamoja na hayo, historia ya ukopaji na namna mhusika anapata kipato ni moja ya mambo muhimu ambayo huangaliwa na wanaokopesha bila dhamana.
Hpo chini ni baadhi ya hatua muhimu za kupata masharti bora zaidi ikiwa unataka kukopa bila dhamana.
Hakikisha mzunguko wa fedha unaeleweka
Ikiwa una historia nzuri ya kukopa na kurudisha pamoja na rekodi yenye nguvu ya uzalishaji wa mapato basi kiwango chako cha riba kitakuwa cha kawaida. Kinyume na hapo, utatozwa kiwango cha juu cha riba katika aina hii ya mkopo. Hivyo ni muhimu kuhakikisha mzunguko wako wa fedha unaeleweka hasa katika siku za mbeleni ambapo kama utachukua mkopo. Kushindwa kulipa mkopo ndani ya muda uliopangwa huleta historia mbaya na kusababisha changamoto ikitokea unahitaji kukopa tena.
Lipa mikopo yako
Lipa mikopo yako ili kukuza historia yako ya ukopaji. Ingawa inawezekana kupata mkopo bila dhamana hata kama una historia mbaya ya ukopaji, unatakiwa kujua kuwa historia mbaya ya ukopaji kutakupelekea kupata viwango vikubwa vya riba katika mkopo usio na dhamana. Jitahidi kulipa mikopo yako kadri uwezavyo ili kupata historia nzuri ya ukopaji na pia hakikisha taarifa zako zote zipo sawa.
Mpango wa biashara ni muhimu
Kama huna mpango wa biashara unashauriwa kutengeneza mpango wako wa biashara kwa sababu wakopeshaji watataka kufahamu kwanini wahatarishe fedha zao kwa kukupatia mkopo, hivyo watataka kujua mtiririko mzima wa fedha katika biashara yako pamoja na mapato ili kujua kama una uwezo wa kulipa mkopo huo au la.
Fanya utafiti kuhusu wakopeshaji
Wakopeshaji wengi tofauti na benki huwa na vigezo vyao, gharama zao na namna yao katika ufanisi wa kazi. Fanya utafiti ili kujua kama mkopeshaji anaendana na malengo yako.
Kupata mkopo katika taasisi tofauti na benki ni rahisi lakini zinaweza kuwa na gharama kubwa zaidi. Ili kurahisisha hilo inashauriwa kujiandaa kama unakwenda kuomba mkopo benki, ili kujipatia masharti na viwango rafiki zaidi.