Home BIASHARA Riba kubwa kikwazo kwa wafanyabiashara

Riba kubwa kikwazo kwa wafanyabiashara

0 comment 89 views

Viwango vya riba hutegemeana na kiasi cha fedha ambacho mkopeshaji humkopesha mkopaji. Katika matukio mengi, kiwango cha riba huhesabiwa kama asilimia ya kila mwaka kulingana na ukubwa wa mkopo. Hivyo ikiwa wewe ni mmiliki wa biashara unatakiwa kujua njia ambazo huathiri viwango vya riba kwani athari yoyote inayotokea huathiri biashara moja kwa moja.

Viwango vya juu vya riba hupunguza mapato kwa watumiaji. Ikiwa viwango vya riba vimeongezeka watumiaji-wenye madeni hulazimika kulipa riba zaidi katika taasisi walizokopa. Hii huleta athari mbaya kwa wakopaji kwa sababu wanalazimika kulipa zaidi hivyo kwenda tofauti na mipango yao.

Viwango vikubwa vya riba huleta ugumu katika biashara kuchukua mikopo. Asilimia kubwa ya biashara hasa ndogondogo huchukua mikopo yenye masharti rafiki ikiwa ni pamoja na riba ndogo hivyo ikiwa viwango vitaongezeka basi mikopo itakuwa ghali, hali ambayo itapelekea wafanyabiashara kushindwa kuchukua mikopo hiyo. Ongezeko la riba husababisha wafanyabiashara wasichukue mikopo kwa kuhofia kushindwa kuilipa.

Viwango vidogo vya riba husababisha watumiaji kukopa fedha zaidi na kuwekeza katika uchumi ikiwa ni pamoja na kutumia mikopo hiyo katika huduma na bidhaa. Hii hurahisisha malipo ya mikopo na kipato hukua kwa namna moja au nyingine kwa sababu mkopaji hutumia fedha za kawaida kulipa gharama za mkopo za kila mwezi huku akiendelea kufanya biashara yake na kutengeneza faida.

Viwango vidogo vya riba huwarahisishia wamiliki wa biashara kuchukua mikopo zaidi kwa ajili ya kuwekeza zaidi na kukuza biashara zao. Kuwa na riba ndogo maana yake mkopo wako utakugharimu fedha ndogo huko mbeleni. Pia viwango vidogo vya riba humaanisha kuwa unaweza kuchukua fedha zilizopo katika biashara na kuzizalisha ili kuongeza kipato zaidi.

Taasisi za fedha zinapaswa kutathmini kwa kina maslahi yao na yale ya wakopaji ili kuhamasisha watu wengi zaidi kukopa. Ukweli ni kwamba watu hupendelea vitu vyenye urahisi hivyo kwa kuweka riba rafiki, wengi watahamasika kukopa, kuwekeza na kukuza uchumi binafsi na wa taifa kwa ujumla.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter