Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Dalili 5 wazo lako sio zuri

Dalili 5 wazo lako sio zuri

0 comment 111 views

Mara nyingi wajasiriamali hujikuta wanawekeza fedha na jitihada kubwa katika wazo la biashara. Wengi husahau hatua muhimu ya kutathmini mawazo yao, hali ambayo inaweza kusababisha hasara kubwa. Kabla ya kuanzisha rasmi kitu fulani jiulize, je wazo hili ni zuri? Biashara hii itanilipa?

Wakati mwingine unaweza kujikuta una wazo zaidi ya moja. Lakini kati ya mawazo hayo lipi lina ubora zaidi na kuna dalili kuwa litazaa matunda? Unapima vipi ubora wa wazo lako kabla ya kuwekeza mali na fedha?

Hizi ni ishara tano kuwa wazo lako sio zuri kama unavyofikiria.

  1. Hakuna uhitaji wa bidhaa au huduma hiyo

Hata kama unafikiri wazo lako ni zuri kiasi gani, kama hakuna uhitaji wa bidhaa au huduma hiyo sokoni basi biashara hiyo haiwezi kufika mbali. Kupima ubora wa wazo ulilonalo, hakikisha tayari wateja wapo sokoni ili unapoingia rasmi kwenye biashara usipoteze muda na fedha nyingi kuwatafuta. Hakuna biashara bila wateja.

  1. Bei ambayo wateja hawawezi kulipa

Biashara nzuri ni mahesabu rahisi; fedha nyingi inatakiwa kuingia kuliko kutoka. Ikiwa hii haitokei mara moja, msimu wake unatakiwa kuwepo kwa muda mfupi tu. Ikiwa wateja wako wanashindwa kunudu bei basi kuna tatizo kwani matumizi yatakuwa makubwa kuliko mapato.

  1. Hakuna wawekezaji

Takribani asilimia 29 ya biashara ndogo hufa kwa sababu zinakosa fedha za kujiendesha. Kila biashara inahitaji fedha. Biashara bila fedha ni kama vile gari bila mafuta, haliwezi kwenda popote. Kwa sababu hiyo, kueleza wazo lako kwa wawekezaji kabla ya kuzindua rasmi biashara yako ni njia nzuri ya kufahamu ubora wa wazo lako. Ukweli ni kwamba kama wazo linashindwa kushawishi wawekezaji kuweka fedha zao basi ni wazi kuwa kuna tatizo.

  1. Bidhaa au huduma zako ni za msimu

Kama kitu ni cha msimu, usijisumbue kukijenga kuwa biashara ya muda mrefu. Badala yake anzisha biashara ndogo ambayo hutegemea na msimu au kitu kinachopendelewa zaidi na wateja kwa wakati huo. Kwa mfano, huwezi kuuza mwamvuli mwaka mzima katika jiji lenye hali ya hewa ya joto kama Dar es salaam na kutegemea kuwa biashara yako itafika mbali.

  1. Wengine wamejaribu na kushindwa

Kama unafikiria kuanzisha biashara ambayo watu wengine wamejaribu kabla yako na kushindwa, jiulize kwanini wewe utafanikiwa? Ni kitu gani kinakutofautisha na ambao wameshindwa hapo awali? Biashara zilizoshindwa zilifanya makosa gani na wewe unachukua hatua gani kuhakikisha kuwa utaepuka makosa hayo? Biashara nyingine kufeli haimaanishi kuwa wazo hilo sio zuri moja kwa moja lakini ni ishara kubwa kuwa unatakiwa kuwa makini, kufahamu soko lako kwa undani na kuwa mbunifu zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter