Kila mtu hutamani kuishi maisha ya ndoto zake na kuachana na masuala ya kufanya kazi kwa watu wengine asubuhi hadi jioni. Kwa mujibu wa utafiti uliofanyika mwaka 2016, asilimia 62 ya watu hufikiria kuanzisha biashara. Utafiti mwingine kuhusu malengo katika kazi uliofanywa na LinkedIn mwaka huo huo ulibaini kuwa 74% ya wafanyakazi wanataka kazi zenye maana.
Hivyo kupitia ripoti hizo ni dhahiri kuwa watu wengi wanatamani kuwa wajasiriamali na kuacha kuripoti kwa watu waliowazidi vyeo. Kufanya kazi kwa ajili yako mwenyewe huleta hamasa zaidi kwa sababu itakubidi ufanye kazi kwa bidii zaidi ili kufanikiwa lakini kufanya maamuzi ya kuacha kazi mapema kunaweza kusababisha ukose kazi na maisha ya ndoto zako.
Unaweza kuwa unataka kuacha kazi kwa sababu unataka uanzishe biashara, usafiri n.k. lakini ni vyema ukijua mambo yafuatayo kabla ya kufanya maamuzi yako.
Kuwa na malengo
Ni muhimu kuwa na maono kuhusu ndoto zako, na namna utakavyoweza kuzitimiza. Ikiwa ni pamoja na kujua jinsi utakavyojijenga, njia ambazo utatumia kupata fedha na kuwekeza katika ndoto zako nk. Jambo la msingi unalotakiwa kukumbuka ni kwamba malengo yatakusaidia kufika pale unapotaka.
Fanya utafiti
Hakikisha unafanya utafiti zaidi kuhusu ndoto yako kabla hujafanya maamuzi ya kuacha kazi na kwenda kuitimiza ndoto hiyo. Siku zote mawazo huwa tofauti na vitendo hivyo fanya utafiti gundua hatari ambazo unaweza kukumbana nazo ikiwa utaamua kutimiza ndoto zako. Hivyo hakikisha unapata ujuzi kadri iwezekanavyo kabla ya kuamua kufanya ndoto yako kwa vitendo, uliza maswali kwa watu ambao tayari wanafanya shughuli kama hiyo.
Andaa mpango wa fedha
Kuwa na mpango wa kifedha ni muhimu ili kuweza kutimiza ndoto zako vinginevyo utapata changamoto ya rasilimali. Ikiwa wewe mwenyewe una mpango wa kujigharamia kifedha ni muhimu kuhakikisha umeweka akiba ya kutosha ili kuweza kuifanya ndoto yako kwa vitendo.
Usiache kazi kwanza
Suala la kuacha kazi na kutimiza ndoto hutamanisha sana lakini ni muhimu kuhakikisha ni muda muafaka wa kufanya hivyo. Inashauriwa kuendelea kufanya kazi huku ukitengeneza njia na mazingira ya kutimiza ndoto yako kwa vitendo. Usikurupuke na kuacha kazi kwasababu kwa namna moja au nyingine kama ndoto zako hazitotimia kama ilivyopangwa nab ado uko kazini hakuna kitakachoharibika, ila kama utaacha kazi na mambo hayatoenda sawa wakati unajaribu kutimiza ndoto zako basi utakosa vyote hivyo kukurudisha nyuma kimaendeleo.
Kuwa na mfuko wa dharura
Ni muhimu kuwa na kiasi cha fedha kwa ajili ya dharura ili hata ukizindua biashara yako na kukawa na mahitaji ya ziada basi iwe rahisi kutatua.
Acha kazi vizuri
Vilevile, ni muhimu kuondoka kazini kwako katika hali nzuri, bila malumbano. Ikiwa kuna mawasiliano mazuri basi ni jambo jema, lakini kama haukuondoka vizuri inaweza kuleta shida.