Ikiwa unafikiria kustaafu mapema unatakiwa kujua kuwa mambo mengi yatabadilika hivyo ni muhimu kujiandaa na kuhakikisha mambo yako yanakwenda sawa, una akiba ya kutosha kumudu matumizi yako kipindi ambacho hutokuwa umeajiriwa.
Zifuatazo ni ishara 5 kuwa upo tayari kustaafu:
Madeni yote yamelipwa
Kama umelipa madeni yako yote basi upo tayari kustaafu kwa sababu baada yakustaafu hautokuwa na mawazo ya jinsi ya kupata fedha kwa ajili ya kulipa madeni badala yake utafurahia maisha na fedha zako ambazo umekuwa ukiziweka kwa ajili ya matumizi kipindi umestaafu. Pia kwa kutokuwa na madeni kutakuepusha kutumia fedha zako za dharura.
Una akiba ya kutosha
Inawezekana ulipanga na kuweka malengo kuhusu akiba wakati wa kustaafu, je uwekezaji wako umetimia na kuzidi kiasi ulichopanga kuweka? Kama ndio basi hiyo ni ishara nzuri kuwa unaweza kustaafu mapema zaidi.
Uwezo wa kumudu masuala ya afya
Muda mwingine huduma za afya zinaweza kuwa na gharama kubwa sana. Hivyo ikiwa una bima nzuri ya afya na mpango madhubuti baada ya kustaafu basi upo tayari kustaafu mapema kwa sababu afya ni muhimu zaidi kabla na hata baada ya kustaafu.
Unaweza kuishi katika bajeti
Baada ya kustaafu ni dhahiri kuwa bajeti itatakiwa zaidi. Mara nyingi inashauriwa kupunguza matumizi na kuweka bajeti ya chini zaidi kuliko ile uliyokuwa nayo wakati unafanya kazi. Jaribu kuweka bajeti ya chini zaidi kwa muda wa mwezi mmoja ili kujua kama unaweza kuimudu. Matokeo utakayoyapata yatakusaidia kujua kama upo tayari au la.
Una mpango mpya
Baada ya kustaafu maisha hubadilika na kunakuwa na umuhimu wa kuweka kipaumbele mambo yasiyohusu kazi. Hivyo jaribu hata wiki moja kuishi kama mstaafu ili kujua kama unaweza kufanya vitu visivyohusu kazi na kuvifurahia. Kama utachoshwa mapema na vitu hivyo basi tambua utakuwa na maisha magumu baada ya kustaafu.