Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Ummy Mwalimu amesema hali ni tete kwenye nafasi za ajira za walimu zilizotangazwa mapema mwezi Mei.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma, waziri Ummy amesema hadi jumapili Mei 23, 2021 maombi ya walimu yalikuwa 89,958 ambapo nafasi zilizotangazwa ni 6,949 pekee.
Alisema “Mheshimiwa spika naomba uiamini serikali, hali ni tete, walioomba na wenye vigezo ni wengi lakini nafasi ni chache, lakini tutatenda haki bila kubagua dini, kabila, jinsia na bila upendeleo wala nafasi ya mtu yeyote.”
Waziri Ummy amesema, pamoja na Wizara kutumia kigezo cha walimu wa kujitolea bado kuna changamoto ya baadhi kughushi barua.
“Ni kweli kigezo kikubwa tunachotumia ni walimu wa kujitolea, lakini kuna malalamiko kuwa kuna wengine wameleta barua feki za kusema wanajitolea wakati hawajitolei,” amesema Ummy.
Amesema “kuna walimu wamemaliza mwaka 2012, 2013, 2014 na 2015 na hawajaajiriwa, upo pia mtazamo ndani ya wizara kuwaangalia hawa waliomaliza siku nyingi wanajitolea na hawajapata ajira.”
Nae Naibu Waziri wa TAMISEMI David Silinde amesema serikali inatamani walimu wote wanaojitolea waajiriwe lakini haitawezekana kutokana na uhaba wa nafasi za ajira.