Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema serikali itaendelea kuzibana kampuni za kigeni ambazo zinashinda tenda za miradi yenye kuleta maendeleo hapa nchini kuajiri watanzania wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo. Waziri Kamwelwe amesema hayo wakati wa uwekaji jiwe la msingi katika ujenzi wa daraja jipya la Selander na barabara unganishi zilizo na urefu wa kilometa 6.23.
“Rais nakuahidi hili nitalisimamia, lakini lingine ni hili la maofisa wa kazi kwenye mikataba hii. Tumeweka Sheria ya kazi ya Tanzania, lakini maofisa kazi wapo kama wanakimbia, tunao katika wilaya na mikoa unamkuta Kamishna wa kazi anahangaika peke yake, hapa pia tungeweza kuongeza mapato”. Amesema Waziri huyo mbele ya Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi na kuongeza:
“Tangu uniteue, yapo maeneo niliyoangalia katika usafirishaji. Kwa mfano, upande wa barabara tuna mabasi 49,000 na kati ya hayo 7,000 yanakwenda mikoani na yaliyobaki ni daladala. Mkoa wa Dar es salaam una daladala 9,000”. Amesema.
Aidha, Waziri huyo amesisitiza kuwa ofisi yake inashirikiana na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato (TRA) ili kuhakikisha serikali inanufaika na mapato yatokanayo na vyombo vya usafiri.