Home AJIRA Unapotafuta masoko, zingatia haya

Unapotafuta masoko, zingatia haya

0 comment 105 views

Si lazima uwe na akili sana ili kuweza kutafuta masoko katika kampuni au biashara, na kuna watu wanafanya kazi hii na hawajawahi kusomea mambo hayo. Kawaida, utayari wa mtu kuhusu kufanya kitu ndio humpelekea mtu huyo kufanikisha na kufanikiwa. Mtu akiwa hafurahii jambo au shughuli anayofanya hawezi kuhamasika sana kufanya kitu hicho na kuhakikisha kinaleta matokeo mazuri.

Basi unaweza kufanya kazi ya masoko ikiwa unaweza haya:

Kutokuwa muoga

Ili kufanya kupata masoko unatakiwa kuwa na uwezo wa kuelezea, kuhamasisha na kushawishi watu kutumia au kununua bidhaa au huduma husika. Uoga unaweza kukufanya usahau jambo ulilotaka kumuelezea mteja, uoga unaweza kukufanya ushindwe hata kutamka maneno jambo linaloweza kupelekea wateja kutotaka kununua bidhaa au biashara kwa sababu hawana taarifa kamili kuhusu bidhaa au huduma hiyo hivyo inakuwa shida kwa wao kujua kama wanahitaji huduma au bidhaa husika. Hivyo basi kama una uwezo wa kujielezea na kuwashawishi watu basi kutafuta masoko inaweza kuwa moja ya kazi ambazo unaweza kufanya.

Kufanya majaribio na kujifunza

Elimu haina mwisho na kila siku maarifa mapya yanatengeneza. Hivyo katika masoko ni muhimu kwenda na wakati ili iwe rahisi kujua watu na mambo wanayopendelea. Hivyo soma vitabu, sikiliza habari n.k. ili uweze kujifunza zaidi na kupitia mambo uliyojifunza fanya majaribio ili kufahamu yamekusaidia kwa kiasi gani na mambo gani unatakiwa kuboresha. Ikiwa unaweza kufanya hivyo na kwa kuwa si muoga basi itakuwa rahisi kutafuta masoko na kufanikiwa.

Kuhudhuria mikutano

Mtu wa masoko hatakiwi kutulia tu, mtu wa masoko anatakiwa kujenga mtandao na hilo linawezekana kwa kukutana na watu wa aina mbalimbali. Ikiwa unafurahia kuhudhulia mikutano mbalimbali na kujichanganya na watu basi kazi ya kutafuta masoko itakufaa. Katika mikutano unaweza usiuze bidhaa au huduma yako, lakini utakutana na watu mbalimbali wenye uelewa na ujuzi tofauti kitu ambacho ni kizuri, kwani utajifunza, utaongeza mawasiliano na kupata mafanikio zaidi.

Ubunifu

Sawa unajifunza kila siku, unafanya majaribio na kupata matokeo, si muoga, swala jingine la muhimu ni ubunifu. Sawa kuna mambo ambayo unatakiwa kuyafuata wakati unatafuta masoko lakini unatakiwa kujiongeza kutokana  na watu unaokutana nao, siku zote huwezi kutumia mbinu moja kwa kila mteja kwani watu hutofautiana. Kama una uwezo wa kufanya mambo kwa njia tofauti basi changamkia fursa katika tasnia ya masoko.

Teknolojia imezidi kurahisisha mambo, siku hizi unaweza kufanya kazi ya masoko kwa kupitia mtandao si lazima ukae ofisini. Hivyo unaweza kufanya kazi ya masoko kama kazi ya kujitegemea (freelance)  huku ukiendelea na shughuli nyingine.

 

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter