Home AJIRA Watumishi 44,000 kuajiriwa serikalini

Watumishi 44,000 kuajiriwa serikalini

0 comment 100 views

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 44,807 katika sekta mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2019/20. Mkuchika amesema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2019/2020 na kutaja baadhi ya sekta hizo kuwa ni pamoja na elimu (13,526), afya (9,467), jeshi la polisi (3,725), kilimo, mifugo na uvuvi (2,141), magereza (685), jeshi la zimamoto na uhamiaji (500), hospitali za mashirika ya dini na hiari (1,262) na vilevile watumishi wapatao 13,002 wa kada nyingine ikiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma.

Pamoja na kutoa ajira, Waziri huyo pia ameeleza kuwa watumishi takribani 290,625 watapandishwa vyeo kulingana na maelekezo yatakayotolewa na kwamba Bodi itafanya utafiti wa hali ya mishahara na maslahi katika vyombo vya ulinzi na usalama ili kushauri mbinu bora zaidi ya kutoa motisha.

“Utoaji motisha utazingatia viwango stahiki vya kuongeza ufanisi katika kazi za vyombo hivyo”. Amesema Mkuchika.

Aidha, Waziri huyo amesema katika kuboresha mazingira kwa watumishi wa umma, Bodi ya Mshahara na Masilahi (Utumishi wa Umma) inaweka tayari taarifa nne za gharama ya maisha zitakazotumika kushauri kiwango cha mshahara unaoendana na gharama halisi za maisha ya watumishi hao.

Akizungumzia uhakiki wa watumishi wa umma, Waziri huyo amesema serikali itahakikisha matumizi mazuri ya rasilimali watu kwa kufanya uhakiki wa watumishi katika sekretariati za mkoa. Ameweka wazi kuwa serikali inachambua madai ya mishahara ya watumishi 21, 683 wanaodai Sh. 50.7 bilioni na kuhakikisha kwamba hatua stahiki zinachukuliwa.

Naye Venance Mwamoto amesema wakati akisoma taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuwa, Kamati hiyo inaunga mkono watumishi wa umma kuongezewa mishahara kwa kuwa gharama za maisha zimekuwa zikiongezeka.

“Sisi sote ni mashahidi kwamba serikali haijaongeza mshahara kwa watumishi wa umma kwa mwaka wa tatu sasa”. Amesema.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter