Benki za CRDB na UBA kwa pamoja zimetoa Sh. 1.7 trilioni (Dola za Marekani milioni 737.5) kwa ajili ya kuidhamini serikali katika mradi wa ujenzi wa umeme wa Rufiji wa Stiegler’s Gorge. Katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika jijini Dar es salaam na kushuhudiwa na waandishi wa habari, watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mkandarasi pamoja na wawakilishi kutoka serikalini, Mkurugenzi Mtendaji wa UBA, Usman Isiaka amesema fedha hizo ni dhamana ya benki inayotakiwa na mkandarasi katika mradi huo utakaogharimu takribani Sh. trilioni 6.6.
“Kwa mujibu wa masharti ya mkataba huo, umoja huo unahitajika kutoa dhamana za benki za kigeni na za ndani zikiwa ni jumla ya Dola za Kimarekani milioni 737.5 kupitia utekelezaji wa mradi na dhamana ya malipo ya awali kwa mradi huo. Kwa kuanzia, Benki ya CRDB na UBA zimeshirikiana na Benki ya Afrika Export-Import (Afrieximbank) na benki nyingine za Misri kutoa dhamana za benki kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambapo sehemu ya dhamana hizo tumezitoa hapa leo (jana)”. Amesema Isiaka.
Mradi wa Stieglers Gorge unatarajia kuiwezesha serikali kukabiliana na tatizo la muda mrefu la upungufu wa umeme kwa kuwa uchumi wa nchi na idadi ya watu inaongezeka.
“Umeme utakaotokana na mradi huu, utatumia kilovolti 400 mpya ambao utaunganishwa katika gridi ya umeme wa taifa”. Amesema.