Home BENKI ACB yatakiwa kuongeza wigo uwekezaji na masoko

ACB yatakiwa kuongeza wigo uwekezaji na masoko

0 comment 95 views

Naibu Waziri wa Fedha, Hamad H Chande ameitaka Benki ya Akiba Commercial (ACB) kuendelea na jitihada za kuongeza wigo wa uwekezaji na masoko nje ya nchi ili kujiimarisha.

Chande ametoa rai hiyo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Akiba Commercial Bank Plc (ACB), Silvest Arumasi, kuhusu fursa za maendeleo ofisini kwake, jijini Dodoma.

Amesema kuwa Sekta ya Benki nchini ikikua, itatoa fursa kwa Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia benki za ndani kuliko kulazimika kwenda kutafuta fedha kwenye benki za nje ambazo hazimnufaishi mwananchi kwa kiwango kikubwa.

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha inakuza sekta ya Benki hususani Benki za Ndani ili kuchochea maendeleo”, amesema Chande.

Aidha, ameihakikishia Benki hiyo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nayo pamoja na Benki nyingine nchini kwa kuwa lengo la Serikali kupitia Wizara ya Fedha ni kuhakikisha sekta ya Benki inaimarika na kutoa mchango katika maendeleo ya nchi.

Amesema Tanzania imeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta ya kibenki katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo yamekuwa na mchango katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Ameipongeza Benki hiyo kwa kuendelea kufanya jitihada za kujimarisha ili kutoa huduma bora kwa wateja wake na Tanzania kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACB Silvest Arumasi, ameipongeza Serikali kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara na akaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwahudumia wananchi.

Amesema kuwa Benki hiyo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwahudumia wajasiriamali wadogo lakini inaendelea na jitihada za kuwafikia watu wengi zaidi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter