Na Mwandishi wetu
Benki ya CRDB imeipatia serikali gawio la bilioni 20, fedha ambazo zilitolewa kama msaada na Mfuko wa Uwekezaji wa Denmark (DIF) mwaka 1996. Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk. Charles Kimei amekabidhi mfano wa hundi hiyo jana kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dk. Dotto James.
Akielezea historia fupi ya msaada huo, Katibu Mkuu wa wizara hiyo amesema serikali ya Denmark ilitoa msaada huo mwaka 1994 kwa lengo la kuisaidia serikali ya Tanzania ili kugharamia uboreshaji wa Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini, ambayo sasa ndiyo CRDB ili kuiwezesha kuboresha huduma zao zaidi.
Serikali ilikuwa na azma ya kufanya benki ya CRDB kuwa na uwezo wa kutoa huduma maalum kwa vyama vya ushirika vya mijini na vijijini hivyo iliwekeza msaada huoya kununua hisa katika benki hiyo.Dk James ameongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa kwenye sekta ya afya ili kunufaisha wananchi na uwekezaj wa serikali katika benki hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB amesema serikali imepatiwa fedha hizo baada ya majadiliano ya siku nyingi kati ya serikali, benki hiyo na bodi ya wadhamini ya DIF. Ameongeza kuwa Bilioni 70 za serikali bado zimebakia kwenye benki hiyo katika akaunti iliyofunguliwa na bodi ya wadhamini baada ya kununua hisa.