Gavana wa Benki kuu ya Tanzania (BoT) Prof. Florens Luoga amesema benki hiyo imekuja na mfumo utakaowatambua wakopaji wote nchini pamoja na taasisi za fedha kufahamu taarifa za wakopaji na vilevile wakopaji nao kujua taarifa zao. Akizundua kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu taarifa za mikopo ya fedha jijini Dar es salaam Prof. Luoga amesema Benki kuu inasimamia uendeshaji wa kanzidata ya taarifa za mikopo pamoja na taasisi zinazoandaa taarifa za mikopo husika.
“Lengo la mfumo huu ni kuwawezesha wakopeshaji kupata taarifa kuhusu tabia za wakopaji ili kujua namna ya kuwahudumia ipasavyo kama wanahitaji mikopo. Ili kuhakikisha usalama wa taarifa za mikopo na kuwalinda walaji au wakopaji, mpango wa kisheria na udhibiti wa taarifa hizo unatoa masharti mahsusi kuhusu ukusanyaji wa taarifa, utoaji wa taarifa na usiri pamoja na kupata idhini kutoka kwa mkopaji ili kutoa taarifa zake za mikopo”. Amefafanua Prof. Luoga
Mfumo huo unatekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kupitia Shirika la Kimataifa la Masuala ya Fedha (IFC), na elimu itatolewa chini ya kaulimbiu “Ifahamu Historia yako ya mikopo, boresha maisha yako”