Mwenyekiti wa umoja wa mabenki Tanzania, Abdulmajid Nsekela amesema benki zimekuwa zikipata changamoto kuwakopesha wachimbaji wadogo kutokana na ukosefu wa leseni na wengine kukodisha jambo ambalo linawafanya washindwe kutambua uhalali wao. Nsekela ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB amesema hayo katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli.
“Wachimbaji hao wamekuwa wakishindwa kufanya upembuzi yakinifu wa mapato yao ambao husaidia benki kutathimini wanachozalisha ili waweze kukopeshwa. Wamekosa mshikamano na umoja ambao ukitiliwa mkazo utaleta matokeo chanya lakini pia wamekuwa wakihamahama jambo ambalo huweka ugumu kwa mabenki kufuatilia utendaji wao. Mabenki yamekuwa yakishiriki katika sekta ya madini katika njia mbalimbali ikiwamo kutoa mikopo kwa wachimbaji mmoja mmoja na wakandarasi na kushiriki katika shughuli mbalimbali. Salio la mikopo iliyotolewa limezidi kukua kutoka Sh. 306 bilioni mwaka 2016 hadi kufikia Sh. 357 bilioni katika mwaka 2018 huku makubaliano yakiwa ni kupelekwa katika shughuli za madini tu”. Ameeleza Nsekela.