Na Mwandishi wetu
Baada ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) kutangaza kuwa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB) ilipata hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 2.4 hivyo kushindwa kujiendesha hali iliyopelekea benki hiyo kufungwa, Chama cha Benki za Kijamii (Cobat) kimedai kuwa uvumi wa kufilisika uliiponza benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Cobat Rukwaro Senkoro amesema baada ya tetesi kuwa MCB itafungwa kusambaa, wateja wengi wa benki hiyo walianza kuhamisha fedha zao. Senkoro ameeleza kuwa benki ya MCB ilikuwa inahitaji milioni 500 tu ili kujikwamua lakini uvumi huo uliiweka benki hiyo ndogo katika nafasi mbaya.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Wanataaluma ya Benki (TIOB) Patrick Mususa amesema madhara ya tetesi kama hizi kwa taasisi ya kifedha yanaweza kudhihirika ndani ya muda mfupi lakini madhara yake huwa ni ya muda mrefu.
Benki kuu ya Tanzania ilitangaza kuifutia leseni ya biashara na kusitisha huduma zote za MCB kutokana na ukosefu wa fedha.